Hakuna hata mtu mmoja aliyenusurika kati ya watu 157 waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka leo asubuhi ikitokea mji mkuu wa Ethiopia Adis Ababa kuelekea Nairobi Kenya.
Raia kutoka mataifa 33 walikuwemo kwenye ndege hiyo yenye nambari ya usajili ET 302 iliyoanguka karibu na mji wa Bishoftu ulioko kiasi kilomita 50 Kusini Mashariki mwa mji mkuu Addis Ababa kwa mujibu wa ripoti.
Msemaji wa shirika la ndege ya Ethiopia ameliambia shirika la habari la kijerumani Dpa, kwamba raia 32 wakenya, Waethiopia 17, na wachina 8 ni miongoni mwa abiria waliokufa waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo. Wamo pia raia kutoka mataifa ya Ufaransa, Italia, Canada, Marekani, Uingereza, Slovakia, Uholanzi, Misri na India.
Ndege aina ya Boeing 737 iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi 8 iliruka mwendo wa saa 8.38 za asubuhi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole na kupoteza mawasiliano dakika chache baadae kwa mujibu wa shirika hilo la ndege la Ethiopia. Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia kwa niaba ya serikali imetowa ujumbe wa salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
Shughuli ya utafutaji miili na uokoaji zinaendelea ingawa imeelezwa kwamba rubani wa ndege hiyo alikabiliana na hitilafu na kutoa taarifa na kisha kuelekezwa kurudi mjini Adis Ababa kwa mujibu wa shirika la ndege.
No comments:
Post a Comment